Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa vyombo vya habari.
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limezuia maandamano ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) yaliyopangwa kufanyika Kesho Novemba 03,2015 katika mji wa Shinyanga kwa lengo la kupinga matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,2015.
Amesema pia wamezuia mikusanyiko yoyote isiyo rasmi ambayo inaweza kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Kamugisha amesema Chadema wametoa taarifa kuwa Kesho wanataka kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25,2015 na baada ya kufanya maandamaano hayo wanataka kutoa ujumbe kwa serikali.
Amewashauri wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga wasishawishiwe na viongozi wa vyama vya siasa,na kuwaomba wabaki majumbani,waendelee na shughuli zao na kutokubali kurubuniwa au kushawishiwa kuandamana kwani wanaowashawishi hawatakuwa mbele .
Katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga mjini George Kitalama amesema hawajapata taarifa wala maelekezo yoyote kuhusu kuzuiwa kwa maandamano yao na wanaendelea kujiandaa na wanachama wao kwa maandamano kama walivyopewa maagizo na viongozi wao wa kitaifa.
Amesema kesho 03.11.2015,watafanya maandamano ya amani kuanzia ofisi za Chadema wilaya kisha kuzunguka mji mzima wa Shinyanga kuanzia saa tatu asubuhi kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume,na kwamba ni maandamano ya nchi nzima siyo Shinyanga pekee.