Mohamed Mwikongi, 'Frank'.
MOHAMMED Mwikongi, maarufu kwa jina la Frank, ni miongoni mwa mastaa wakali wa kitambo kwenye tasnia ya sanaa ya maigizo hapa nchini.Alianza kutikisa kwenye anga la sanaa hiyo akiwa kwenye Kundi la Kaole Sanaa ambalo kwa sasa linajulikana kama Kaone, kabla ya kuhamia kwenye filamu.
staa huyu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu akiwa kama mmoja wa wadau wanaopenda siasa, ameamua kujitosa katika kugombea ubunge kwenye Jimbo la Segerea lililopo Tabata jijini Dar es Salaam kupitia Chama cha ACT–Wazalendo.Championi Jumatatu linakuletea kilingeni mkali huyu kwa ajili ya mahojiano maalumu.
Kwa nini uliamua kuingia kwenye siasa?
Nikiwa kama kijana ambaye ninajiamini, nimeona huu ndiyo wakati wangu muafaka wa kuingia katika siasa, lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa kero hasa katika jamii inayotuzunguka, ili kuzitolea ufumbuzi, hasa ukosefu wa ajira na uchumi.
Utafanya nini kuhakikisha unashinda katika uchaguzi huo?
Sera na fikra zangu yakinifu ndizo zitakazowafanya Wana-Segerea wanielewe hasa pale nitakapotoa mawazo yangu chanya kwa kuzingatia ushirikiano, umoja pamoja na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau, yatakayoleta nguvu na utekelezaji wa sera zitakazoweza kuleta maendeleo.
Zipi kero utakazotatua hapo Segerea endapo utashinda?
Kwa pamoja mimi na Wana-Segerea baada ya kunichagua, tutahakikisha tunatengeza fursa za ajira za kutosha, nitasimamia kurekebisha miundombinu ikiwemo barabara pamoja na maji.
Unawazungumziaje wagombea ambao wanahamahama vyama?
Hiyo ni dalili mbaya sana, hasa kwenye vyama walivyoenda, lakini pia wanakosa uzalendo na uadilifu.
Historia ya siasa kwenye familia yako ipoje?
Huwezi amini, hakuna hata mtu mmoja ambaye amewahi kuitumikia siasa, ndiyo maana ninasema wakati wangu wa kuleta mabadiliko katika jamii umefika kwa sababu ingekuwa ni kufuata mkumbo au kufanya siasa kwa ushawishi basi ningewaangalia ndugu zangu, lakini haipo hivyo.
Unawaambia nini wasanii walioanguka katika kura za maoni?
Hakuna kukata tamaa kwani matumaini bado yapo na mapambano yanaendelea, hivyo ni vyema nidhamu na busara vikachukua nafasi katika vyama vyao kwani lolote linaweza kutokea mbele.
Utawezaje kumudu siasa na sanaa kwa wakati mmoja?
Ni kama ilivyo mafuta na maji, kwa kweli siasa siyo suala la mchezo na kwa kuwa ninaiheshimu jamii pamoja na nchi yangu, sanaa nitaipisha kidogo ili niweze kuwatumikia Wana-Segerea, hata hivyo nitakuza vipaji kwa vijana wadogo katika kuanzisha akademi mbalimbali zinazohusu sanaa na michezo kwa ujumla.
Utaifanyia nini tasnia ya maigizo kama ukipata ubunge?
Nitapigania haki za msingi kuhakikisha zinaonekana, hasa fursa ya kutangaza sanaa zetu na kupunguza vikwazo vinavyofanya sanaa yetu ishuke na kupoteza baadhi ya majina ya watu maarufu.
Neno la mwisho
Sote kwa pamoja tushikamane, tupeane hamasa, hasa kipindi hiki cha uchaguzi, pamoja na kumuomba Mungu mambo yaende sawa kwani shetani naye anaweza kuingilia kati mambo yakakwama, wakati kila mmoja anajua Tanzania ni nchi yenye amani.