Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Kilimanjaro imeteketeza lita 140 za gongo, mapipa 40 na mitambo sita ya kutengeneza pombe hiyo haramu vyenye thamani ya Sh10 milioni.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Rombo
Alisema mitambo hiyo ya gongo iliteketezwa katika kijiji cha Kikelelwa Tarakea wilayani humo.
Makala alisema pombe hiyo imekuwa ikileta madhara kwa wananchi hasa vijana ambao wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na kunywa muda wa kazi
Alisema wilaya hiyo inaongoza kwa kutengeneza pombe za kenyeji zaidi ya 50 kwa kutumia kemikali hatarishi.
"Gongo inaathari kubwa kutokana na utengenezaji wake, nimeambiwa wanaweka maji ya betri na kinyesi cha binadamu,” alisema Makala.
Alisema pombe hiyo inatajwa kuharibu nguvu za kiume na kupoteza nguvu kazi kubwa kwa Taifa hali inayosababisha kazi za wanaume kufanywa na wanawake.
Awali, kamati hiyo ya ulinzi na usalama ilikagua mipaka ya Kenya na Tanzania kuanzia Holili hadi Tarakea.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo Lembris Kipuyo, alisema anapambana kukomesha unywaji wa pombe saa za kazi na utengenezaji wa pombe hizo.
Alisema wataendelea kukamata mitambo pamoja na malighafi za kutengeneza pombe hizo
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mh. Amos Makalla na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na usalama Mkoa wakikagua mpaka wa Tanzania na Kenya